Watoto yatima na malezi ya kiakili/kisaikolojia

WATOTO yatima, waliofiwa na mzazi mmoja au wote wawili, ni kundi linaloongezeka kwa kasi kubwa, hasa Afrika na sababu kubwa ni janga la Ukimwi. Bado tuna hatua ya kupiga katika mapambano dhidi ya ukimwi katika sura nyingi, lakini sura hii ya watoto yatima inatulazimu kutafuta mbinu mpya kila wakati ili kukabili matatizo wanayopata.

Kutokana na mila na desturi, familia nyingi za Afrika zimetunza watoto yatima, pamoja na ukweli kwamba njia hii pia imeelemewa, ukizingatia ugumu wa maisha kwa familia nyingi (umaskini) na hivyo kuwa ni njia ambayo imekuwa na changamoto nyingi. Leo ningependa kuzungumzia suala la watoto yatima kutunzwa katika familia zetu na kuhusisha suala la kuwatunza kimwili na kuwapa mapenzi na msaada zaidi ya mahitaji ya kimwili, kama chakula, malazi, mavazi na mahitaji mengine.

Familia nyingi humtunza mtoto kimwili na kusahau kwamba mtoto yatima anahitaji zaidi mapenzi na uwepo wa huduma ya kisaikolojia au kiakili ili kumsaidia kupita katika kipindi hicho kigumu cha kupoteza mzazi/wazazi. Wataalamu wanasema kwamba kipindi mzazi anapougua, mtoto hupitia wakati mgumu, kimawazo na kisaikolojia, maumivu ya kiroho yanayoambatana na mawazo ya ni jinsi gani ataishi bila mzazi huyo pale atakapoaga dunia humsumbua akili.

Katika hali ya kawaida, mtoto yeyote huhitaji uwepo wa mzazi katika maisha yake. Katika kipindi hiki ndugu na jamaa huwa karibu katika kutoa msaada wa kimwili zaidi kuliko wa kisaikolojia na kiakili hivyo mtoto kupungukiwa kwa kiasi kikubwa na ulinzi katika eneo la makuzi kisaikolojia.

Mzazi anapofariki, watoto hupitia kipindi kigumu zaidi, kwa vile yale mapenzi ya mzazi na ule uhakika wa kuishi kwa matumaini makubwa, hata kama alikuwa ni maskini hupungua. Nuru iliyokuwepo katika maisha yake hupotea ghafla. Malezi yale ya kisaikolojia aliyokuwa akipata kutoka kwa mzazi hupotea na katika kipindi hiki, hali ya mtoto ya kisaikolojia na kihisia huwa katika kipindi kigumu zaidi.

Hali hii si tu ya kipindi ambacho amefariki mzazi, bali huambatana na maisha katika makuzi yake yote kwa vile watoto huhitaji uwepo wa wazazi wao katika kipindi chote cha makuzi yao.

Watoto ambao wazazi wao wamefariki kwa Ukimwi huwa katika hali tete zaidi, kwa vile hunyanyapaliwa katika ngazi ya familia na hata jamii. Hali hii humwongezea mtoto huzuni na simanzi na kama hapati msaada wa kisaikolojia au kiakili huwa katika hali tete kisaikolojia. Watoto hawa huhitaji mtu anayeaminika wa karibu wa kumweleza matatizo yao, hisia zao bila woga wa kunyanyapaliwa au kutengwa au kubaguliwa.

Mtu huyu ni lazima awe msikivu, mwelewa na mwenye msaada kwa mtoto. Hili ni jambo ambalo walezi wote wajitahidi kulitimiza kwa vile si tu kwamba ni wajibu wa mlezi, bali huokoa maisha ya sasa na mbeleni ya mtoto yatima.

Ni vyema pia kukumbuka kwamba utoaji wa huduma ya kisaikolojia kwa mtoto huendana na umri na mtoto mwenyewe. Watoto hutofautiana namna wanavyokabili changamoto za kupotelewa mzazi na vilevile, umri pia ni kigezo cha namna ya kutoa huduma hii.Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s