Mafanikio ya watoto yatima na elimu

Watoto yatima ni kama watoto wengine na wanahaki ya kupata elimu ya kutosha/sawa kama wanavyopata watoto wenye wazazi na sio kubaguliwa.Kwasababu kuna baadhi ya wanajamii wanabagua watoto yatima na kusema hawapaswi kusoma katika shule nzuri na hatimaye kupelekwa katika shule za kawaida lakini watoto wenye wazazi ndio wanopaswa kusoma katika shule zenye uwezo.

Elimu ni suala la watu wote na sio kubaguliwa na kusema watoto yatima hawawezi kujimudu kielimu katika shule za msingi,sekondari,mpaka chuo kikuu ila elimu wanayopaswa kupewa watoto yatima ni zile elimu za kiufundi kama ushonaji nk.

Advertisements

Watoto wa mitaani na mazingira

Imeelezwa kuwa kuna sababu nyingi zinazochangia kuwepo kwa watoto wa mitaani na wale wanaoishi katika mazingira magumu hapa nchini, huku sababu kuu ikielezwa kwamba ni kuanguka kwa uchumi katika familia nyingi.

Watoto kwenye mazingira magumu.

Bado kuna msaada mkubwa unotakiwa kutolewa na jamii,serikari kutokomeaza suala zima la watoto wa mitaani na hawapati misaada kwa jamii na kujishughulisha wenyewe na biashara ndogondogo.


Chanzo cha watoto wa mitaani

WAKATI  nchi za Afrika zilipofanya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Juni 16 ikiwa ni njia mojawapo ya kuwakumbuka na kuwaenzi watoto wa Afrika Kusini ambao walifanyanyaswa na kubaguliwa na hata kuuawa wakati wa ubaguzi wa rangi, Tanzania inaelezwa kuwa haina takwimu sahihi za watoto wa mitaani.

Kukosekana kwa takwimu hizo kumeelezwa kuwa kunatokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuongezeka siku hadi siku kila sehemu kwa watoto hao, hali ambayo inawafanya watendaji wa Serikali wakose takwimu hizo.Pia, inaelezwa kwamba watoto wengine wanaishi katika mazingira magumu  na hatarishi kwa afya zao, lakini bila kutambuliwa.

Wakiwa mitaani huko, watoto hao wamekuwa wakikumbana na mambo mbalimbali yakiwamo kubakwa, kunyanyaswa, kudhalilishwa kijinsia, vitendo wanavyofanyiwa na watu mbalimbali wakiwamo watoto wenzao na hata watu wazima.

Ugomvi wa wazazi kwenye familia,kutowajibika ipasavyo na umaskini ni  sababu mojawapo ya zinazofanya watoto hao kutoroka na kuingia mitaani na kuishi katika mazingira magumu, hali ambayo inaonyesha wazi kuwa, jamii imeshindwa kuwajibika ipasavyo.Watoto hao ambao wanategemewa kuwa viongozi wa baadaye, lakini wanaonekana kuwa na maisha magumu yanayosababisha kukosa elimu, malezi bora jambo ambalo linawafanya waishi katika mazingira hatarishi.

Ili kutatua tatizo hilo, Serikali, jamii na wadau mbalimbali zikiwamo taasisi za kiraia zina wajibu wa kushirikiana  kwa pamoja na ili kuhakikisha kuwa, wanatoa elimu kuhusu suala hilo.Mbali na wadau hao, walimu pia wana nafasi kubwa ya kutoa elimu kwa wazazi na wanafunzi kupiga vita suala la kutupwa watoto,unyanyasaji, ubebaji wa mimba bila ya kujiandaa jambo ambalo linaweza kupunguza kama si kumaliza  tatizo hilo.


Watoto wa mitaani

Watoto wa mitaani ni watoto kama wengine na wanahaki sawa kama watoto wengine.Lakini kuna baadhi ya wanajamii wanabagua sana watoto wa mitaani na kuwapa kipaumbele sana watoto wa majumbani.

Pia wa mitaani ni moja ya makundi yanayokosa huduma muhimu kutoka kwa jamii. Watoto hao pia wapo kwenye hatari kubwa ya kutendewa vitendo viovu vya udhalilishaji na kuambukizwa virusi vya Upungufu wa Kinga Mwilini (Ukimwi).

Imekuwa kawaida katika jamii, kuwaita watoto hawa kuwa “watoto wa mitaani”, wakati mitaa haizai watoto. Watoto wengi hukimbia nyumbani kwa wazazi wao, kutokana na kukosa huduma, kunyanyaswa na wanafamilia, hasa wazazi wa kambo.

Swali la kujiuliza; kwa nini watoto hao huondoka majumbani mwao?

Watoto wengi wanaeleza sababu mbalimbali zinazofanya watoto hao kukimbilia mitaani, ambazo ni: kukataliwa na baba au mama zao wa kambo, kufiwa na wazazi na kupigwa. Wengine hutumika kama vitega uchumi vya wazazi, hasa wanaoishi mijini.

Wapo watoto wa mitaani waliofiwa na wazazi. Lakini wajomba, shangazi na ndugu wengine, hugoma kuwachukua au kuwalea watoto hao, kutokana na hali ya uchumi, ambayo husababisha wakimbilie mitaani ili kupata walau fedha za kujikimu.

Baadhi ya watoto wa mitaani kukidhi mahitaji yao wenyewe.


Watoto yatima na mazingira ya kifamilia/majumbani

Wataalam wa maswala ya watoto na makuzi yao, wanabainisha kwamba; watoto yatima wanapaswa kusaidiwa kwa kubaki katika mazingira na maisha ya kifamilia zaidi. Kuhakikisha kwamba wanapata mahitaji yao msingi; fursa za masomo ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea kwa siku za usoni, pamoja na kuwapatia ushauri nasaha na mambo ya kisaikolojia ili waweze kukabiliana na uhalisi wa maisha, badala ya kuishi katika ndoto, hali ambayo inaweza kuwafanya kukata tamaa na hivyo kukosa mwelekeo wa maisha.

Watoto wengi yatima ambao wameondokewa na wazazi na walezi wao, wanajikuta wakilelewa na Bibi na Babu zao au ndugu wa familia, hali hii inayoendelea kujenga uhusiano mwema kati ya watoto na jamii husika, kuliko tabia na mwelekeo wa watu wengi kutaka kuwapeleka watoto hawa katika vituo vya kutunza na kulelea watoto yatima.
Wazazi, kimsingi wanapaswa kuhakikisha kwamba wanaacha wosia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto wao, kwani mara nyingi watoto yatima wamejikuta wakiporwa hata ule urithi kidogo walioachiwa na wazazi wao.

Wataalam hawa wanakiri kwamba; hali ngumu ya uchumi na ukata wa maisha kwa ujumla, unafanya ndugu wengi kutaka kuwapeleka watoto yatima kwenye vituo vya kutunza na kulea yatima, kutokana na uhalisi wa maisha yenyewe na changamoto wanazokabiliana nazo katika haja ya maisha yao ya kila siku. Walezi hawa pia wanapaswa kusaidiwa na wataalam wa masuala ya kisaikolojia ili waweze kuipokea na kukubali hali waliyo nayo kwaajili ya mafao ya watoto yatima.

Mara nyingi walezi wa watoto yatima, wengi wao hawapati ushauri wala msaada wa kijamii kama ambavyo ingepaswa kufanyika, hali inayowatendea hata watoto yatima wanapoishi katika mazingira kama haya. Walezi wa watoto yatima wahakikishe kwamba wanapewa ushauri wa kisaikolojia ili kupambana vyema na uhalisi wa maisha, kwa kuwahimiza kuwapeleka watoto yatima shuleni badala ya kuwaficha majumbani kwao, kisingizio cha ukata na hali ngumu ya maisha. Watoto yatima wakiwezeshwa katika elimu, wanaweza kufanya maajabu katika maisha yao ya  baadae.


Watoto yatima na malezi ya kiakili/kisaikolojia

WATOTO yatima, waliofiwa na mzazi mmoja au wote wawili, ni kundi linaloongezeka kwa kasi kubwa, hasa Afrika na sababu kubwa ni janga la Ukimwi. Bado tuna hatua ya kupiga katika mapambano dhidi ya ukimwi katika sura nyingi, lakini sura hii ya watoto yatima inatulazimu kutafuta mbinu mpya kila wakati ili kukabili matatizo wanayopata.

Kutokana na mila na desturi, familia nyingi za Afrika zimetunza watoto yatima, pamoja na ukweli kwamba njia hii pia imeelemewa, ukizingatia ugumu wa maisha kwa familia nyingi (umaskini) na hivyo kuwa ni njia ambayo imekuwa na changamoto nyingi. Leo ningependa kuzungumzia suala la watoto yatima kutunzwa katika familia zetu na kuhusisha suala la kuwatunza kimwili na kuwapa mapenzi na msaada zaidi ya mahitaji ya kimwili, kama chakula, malazi, mavazi na mahitaji mengine.

Familia nyingi humtunza mtoto kimwili na kusahau kwamba mtoto yatima anahitaji zaidi mapenzi na uwepo wa huduma ya kisaikolojia au kiakili ili kumsaidia kupita katika kipindi hicho kigumu cha kupoteza mzazi/wazazi. Wataalamu wanasema kwamba kipindi mzazi anapougua, mtoto hupitia wakati mgumu, kimawazo na kisaikolojia, maumivu ya kiroho yanayoambatana na mawazo ya ni jinsi gani ataishi bila mzazi huyo pale atakapoaga dunia humsumbua akili.

Katika hali ya kawaida, mtoto yeyote huhitaji uwepo wa mzazi katika maisha yake. Katika kipindi hiki ndugu na jamaa huwa karibu katika kutoa msaada wa kimwili zaidi kuliko wa kisaikolojia na kiakili hivyo mtoto kupungukiwa kwa kiasi kikubwa na ulinzi katika eneo la makuzi kisaikolojia.

Mzazi anapofariki, watoto hupitia kipindi kigumu zaidi, kwa vile yale mapenzi ya mzazi na ule uhakika wa kuishi kwa matumaini makubwa, hata kama alikuwa ni maskini hupungua. Nuru iliyokuwepo katika maisha yake hupotea ghafla. Malezi yale ya kisaikolojia aliyokuwa akipata kutoka kwa mzazi hupotea na katika kipindi hiki, hali ya mtoto ya kisaikolojia na kihisia huwa katika kipindi kigumu zaidi.

Hali hii si tu ya kipindi ambacho amefariki mzazi, bali huambatana na maisha katika makuzi yake yote kwa vile watoto huhitaji uwepo wa wazazi wao katika kipindi chote cha makuzi yao.

Watoto ambao wazazi wao wamefariki kwa Ukimwi huwa katika hali tete zaidi, kwa vile hunyanyapaliwa katika ngazi ya familia na hata jamii. Hali hii humwongezea mtoto huzuni na simanzi na kama hapati msaada wa kisaikolojia au kiakili huwa katika hali tete kisaikolojia. Watoto hawa huhitaji mtu anayeaminika wa karibu wa kumweleza matatizo yao, hisia zao bila woga wa kunyanyapaliwa au kutengwa au kubaguliwa.

Mtu huyu ni lazima awe msikivu, mwelewa na mwenye msaada kwa mtoto. Hili ni jambo ambalo walezi wote wajitahidi kulitimiza kwa vile si tu kwamba ni wajibu wa mlezi, bali huokoa maisha ya sasa na mbeleni ya mtoto yatima.

Ni vyema pia kukumbuka kwamba utoaji wa huduma ya kisaikolojia kwa mtoto huendana na umri na mtoto mwenyewe. Watoto hutofautiana namna wanavyokabili changamoto za kupotelewa mzazi na vilevile, umri pia ni kigezo cha namna ya kutoa huduma hii.


Michango ya watoto yatima katika jamii

JAMII imetakiwa kutambua umuhimu wa kuwatunza na kuwalea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia haki zao za msingi ikiwemo elimu vyakula na mavazi.
Wito huo umetolewa na mbunge viti maalum mkoa mpya wa Geita Mh.Vick-Kamata alipotembelea vituo vya kulelea watoto yatima vya Moyo wa Huruma chenye watoto 84 na Lelea chenye watoto 25 vilivyopo wilayani Geita sanjari na kutoa msaada wenye thamani ya shilingi milioni 3 wa vyakula,mavazi na vinywaji kwa watoto hao ili kuwawezesha kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya 2011.


Amesema kuwa ili kuondoa wimbi la watoto wanaoishi mitaani jamii haina budi ya kuwa inajukumu kubwa la kuwatunza,kuwalea  na kuwawezesha kupata elimu itayowasaidia kujikwamua katika maisha yao ya baadae.
Mh.Kamata ametoa msaada wa mafuta ya kupikia lita 60,Sabuni za kufulia,vinyaji,mchele kilo 200,mbuzi wawili,madaftari kalamu na sukari ambapo pia alishiriki na watoto hao kula nao chakula cha mchana katika kusherehekea mwaka mpya.
Kadharika mbunge huyo ametoa pia msaada wa nguo,Unga wa lishe kwa wafungwa na mahabusu wakiwemo watoto wane ambao mamazao wamo katika gereza la Geita pamoja na kuzungumza na wafungwa na mahabusu wa gereza hilo ambapo amejionea msongamo wa mahabusu unaotokana na kucheleweshwa kwa upelezi wa kesi zinazowakabili.
Aidha kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Geita Joseph Msukuma amesema wilaya hiyo inakabiliwa na ongezeko la idadi ya watoto wanaoishi mitaani hali inayotokana na kuongezeka kwa msongamano wa watu katika Mji wa Geita.
Mwenyekiti ameyataka mashirika hayo yanayolea watoto yatima kufanya jitihada za makusudi kwa kushirikiana na Serikali wahisani na mashirika mbalimbali kuwaondoa watoto walioko mitaani na kuwaweka pamoja ili kuweza kuwalea na kuwapatia elimu itayowasaidia  hapo baadae.
Katika kuunga mkono juhudi za mashirika hao za kulea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu mwenyekiti huyo ametoa msaada wa magodoro 25.Mkoa mpya wa Geita unakabiliwa na ongezeko la watoto wa mitaani ambapo zaidi ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu 2000 wanaishi mitaani kutokana na kuongezeka idadi ambapo zaidi ya watu 100,000 wanaishi mjini Geita.