Watoto yatima waliokuwa mitaani

Watoto yatima ni miongoni mwa watoto ambao waliofiwa na wazazi wote wawili.Na hata mzazi mmoja wanaoishi katika mazingira magumu majumbani na hatimaye kutoroka na kwenda mitaani kutafuta maisha yao wenyewe.

Kutokana na malezi ya wazazi waliobakia na majukumu ya kulea watoto ambao wamefiwa na wazazi wao kuwapelekea maisha kuwa magumu na kushindwa kukidhi maitaji ya watoto wote haliokuwa nao inasababisha baadhi ya watoto kubaguliwa katika familia hiyo.

John Erick ni mmoja wa watoto yatima wanoishi mitaani amesema”Kutokana na wazazi wangu wote kufariki dunia  na kutokuishi vizuri na walezi wangu ninaoishi nao ndio sababu iliyonipelekea mimi kuishi mitaani na kuondoka kwetu, ni bora nihishi mitaani kuliko kukaa na mlezi wangu kwa sababu ata chakula ninakosa,shule siendi,na hata pa kulala ni chumba kimoja si maadili ya kitanzania.”

Bwana Abdalah Bakari mmoja wa wanajamii amesema kama jamii itakuwa imeelimika vizuri  juu ya huduma ya mtoto, na pia kuendeleza moyo wa kujitolea kwa uwangalizi wa vijana, hakutakuwa na kukabiliwa na tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Amesema watoto huhitajika upendo na huruma, sifa mbili muhimu ambazo yatima anazikosa, zinazowalazimisha wao kupata kimbilio kwenye mitaa, hivyo kuishia kuwa watoto wa mitaani.

Abdalah alisema serikali peke yake haiwezi kushughulikia watoto peke yake, na kuongeza kwamba kutunza watoto kuna kwenda sambamba na kuwapa elimu na kanuni za malezi kama watoto wengine wanaoishi na familia zao.

“Wito wangu kwa jamii ni kupata motisha na kutoa misaada yao kwa vile serikali peke yake haiwezi kufanya hivyo,”alisema.

 

 


Maisha ya watoto yatima waliokosa muongozo

Watoto yatima ni watoto kama watoto wengine,na wanayo nafasi katika jamii  kujaliwa na kupewa huduma kama watoto wengine,lakini bado kuna watoto yatima ambao wanabaguliwa na hawapati huduma za kutosha kama mtoto.

Asha Bakari ni miongoni mwa watoto yatima ambao anaishi katika maisha magumu apati huduma zinazotakiwa mtoto kuzipata,anesema muda mwingi anatumia kufanya kazi za nyumbani na kulea mtoto wa baba yake mkubwa.

Amesema kila atakapo mueleza baba yake mkubwa suala la kwenda shule anmgombeza na kumwambia kazi yake yeye ni kulea na kufanya kazi za nyumbani ili baadae hadumu kwenye ndoa yake.

Kwa hiyo bado kuna baadhi ya jamii wanaobagua watoto yatima katika familia na kutoa muongozo mbaya wa maisha yake ya baadae.Wanajamii tunatakiwa kubadilika na kuwa na upendo na umoja kwa watoto yatima kwa ujumla.


Mafanikio ya watoto yatima na elimu

Watoto yatima ni kama watoto wengine na wanahaki ya kupata elimu ya kutosha/sawa kama wanavyopata watoto wenye wazazi na sio kubaguliwa.Kwasababu kuna baadhi ya wanajamii wanabagua watoto yatima na kusema hawapaswi kusoma katika shule nzuri na hatimaye kupelekwa katika shule za kawaida lakini watoto wenye wazazi ndio wanopaswa kusoma katika shule zenye uwezo.

Elimu ni suala la watu wote na sio kubaguliwa na kusema watoto yatima hawawezi kujimudu kielimu katika shule za msingi,sekondari,mpaka chuo kikuu ila elimu wanayopaswa kupewa watoto yatima ni zile elimu za kiufundi kama ushonaji nk.


Watoto yatima na mazingira ya kifamilia/majumbani

Wataalam wa maswala ya watoto na makuzi yao, wanabainisha kwamba; watoto yatima wanapaswa kusaidiwa kwa kubaki katika mazingira na maisha ya kifamilia zaidi. Kuhakikisha kwamba wanapata mahitaji yao msingi; fursa za masomo ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea kwa siku za usoni, pamoja na kuwapatia ushauri nasaha na mambo ya kisaikolojia ili waweze kukabiliana na uhalisi wa maisha, badala ya kuishi katika ndoto, hali ambayo inaweza kuwafanya kukata tamaa na hivyo kukosa mwelekeo wa maisha.

Watoto wengi yatima ambao wameondokewa na wazazi na walezi wao, wanajikuta wakilelewa na Bibi na Babu zao au ndugu wa familia, hali hii inayoendelea kujenga uhusiano mwema kati ya watoto na jamii husika, kuliko tabia na mwelekeo wa watu wengi kutaka kuwapeleka watoto hawa katika vituo vya kutunza na kulelea watoto yatima.
Wazazi, kimsingi wanapaswa kuhakikisha kwamba wanaacha wosia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto wao, kwani mara nyingi watoto yatima wamejikuta wakiporwa hata ule urithi kidogo walioachiwa na wazazi wao.

Wataalam hawa wanakiri kwamba; hali ngumu ya uchumi na ukata wa maisha kwa ujumla, unafanya ndugu wengi kutaka kuwapeleka watoto yatima kwenye vituo vya kutunza na kulea yatima, kutokana na uhalisi wa maisha yenyewe na changamoto wanazokabiliana nazo katika haja ya maisha yao ya kila siku. Walezi hawa pia wanapaswa kusaidiwa na wataalam wa masuala ya kisaikolojia ili waweze kuipokea na kukubali hali waliyo nayo kwaajili ya mafao ya watoto yatima.

Mara nyingi walezi wa watoto yatima, wengi wao hawapati ushauri wala msaada wa kijamii kama ambavyo ingepaswa kufanyika, hali inayowatendea hata watoto yatima wanapoishi katika mazingira kama haya. Walezi wa watoto yatima wahakikishe kwamba wanapewa ushauri wa kisaikolojia ili kupambana vyema na uhalisi wa maisha, kwa kuwahimiza kuwapeleka watoto yatima shuleni badala ya kuwaficha majumbani kwao, kisingizio cha ukata na hali ngumu ya maisha. Watoto yatima wakiwezeshwa katika elimu, wanaweza kufanya maajabu katika maisha yao ya  baadae.


Watoto yatima na malezi ya kiakili/kisaikolojia

WATOTO yatima, waliofiwa na mzazi mmoja au wote wawili, ni kundi linaloongezeka kwa kasi kubwa, hasa Afrika na sababu kubwa ni janga la Ukimwi. Bado tuna hatua ya kupiga katika mapambano dhidi ya ukimwi katika sura nyingi, lakini sura hii ya watoto yatima inatulazimu kutafuta mbinu mpya kila wakati ili kukabili matatizo wanayopata.

Kutokana na mila na desturi, familia nyingi za Afrika zimetunza watoto yatima, pamoja na ukweli kwamba njia hii pia imeelemewa, ukizingatia ugumu wa maisha kwa familia nyingi (umaskini) na hivyo kuwa ni njia ambayo imekuwa na changamoto nyingi. Leo ningependa kuzungumzia suala la watoto yatima kutunzwa katika familia zetu na kuhusisha suala la kuwatunza kimwili na kuwapa mapenzi na msaada zaidi ya mahitaji ya kimwili, kama chakula, malazi, mavazi na mahitaji mengine.

Familia nyingi humtunza mtoto kimwili na kusahau kwamba mtoto yatima anahitaji zaidi mapenzi na uwepo wa huduma ya kisaikolojia au kiakili ili kumsaidia kupita katika kipindi hicho kigumu cha kupoteza mzazi/wazazi. Wataalamu wanasema kwamba kipindi mzazi anapougua, mtoto hupitia wakati mgumu, kimawazo na kisaikolojia, maumivu ya kiroho yanayoambatana na mawazo ya ni jinsi gani ataishi bila mzazi huyo pale atakapoaga dunia humsumbua akili.

Katika hali ya kawaida, mtoto yeyote huhitaji uwepo wa mzazi katika maisha yake. Katika kipindi hiki ndugu na jamaa huwa karibu katika kutoa msaada wa kimwili zaidi kuliko wa kisaikolojia na kiakili hivyo mtoto kupungukiwa kwa kiasi kikubwa na ulinzi katika eneo la makuzi kisaikolojia.

Mzazi anapofariki, watoto hupitia kipindi kigumu zaidi, kwa vile yale mapenzi ya mzazi na ule uhakika wa kuishi kwa matumaini makubwa, hata kama alikuwa ni maskini hupungua. Nuru iliyokuwepo katika maisha yake hupotea ghafla. Malezi yale ya kisaikolojia aliyokuwa akipata kutoka kwa mzazi hupotea na katika kipindi hiki, hali ya mtoto ya kisaikolojia na kihisia huwa katika kipindi kigumu zaidi.

Hali hii si tu ya kipindi ambacho amefariki mzazi, bali huambatana na maisha katika makuzi yake yote kwa vile watoto huhitaji uwepo wa wazazi wao katika kipindi chote cha makuzi yao.

Watoto ambao wazazi wao wamefariki kwa Ukimwi huwa katika hali tete zaidi, kwa vile hunyanyapaliwa katika ngazi ya familia na hata jamii. Hali hii humwongezea mtoto huzuni na simanzi na kama hapati msaada wa kisaikolojia au kiakili huwa katika hali tete kisaikolojia. Watoto hawa huhitaji mtu anayeaminika wa karibu wa kumweleza matatizo yao, hisia zao bila woga wa kunyanyapaliwa au kutengwa au kubaguliwa.

Mtu huyu ni lazima awe msikivu, mwelewa na mwenye msaada kwa mtoto. Hili ni jambo ambalo walezi wote wajitahidi kulitimiza kwa vile si tu kwamba ni wajibu wa mlezi, bali huokoa maisha ya sasa na mbeleni ya mtoto yatima.

Ni vyema pia kukumbuka kwamba utoaji wa huduma ya kisaikolojia kwa mtoto huendana na umri na mtoto mwenyewe. Watoto hutofautiana namna wanavyokabili changamoto za kupotelewa mzazi na vilevile, umri pia ni kigezo cha namna ya kutoa huduma hii.


Michango ya watoto yatima katika jamii

JAMII imetakiwa kutambua umuhimu wa kuwatunza na kuwalea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia haki zao za msingi ikiwemo elimu vyakula na mavazi.
Wito huo umetolewa na mbunge viti maalum mkoa mpya wa Geita Mh.Vick-Kamata alipotembelea vituo vya kulelea watoto yatima vya Moyo wa Huruma chenye watoto 84 na Lelea chenye watoto 25 vilivyopo wilayani Geita sanjari na kutoa msaada wenye thamani ya shilingi milioni 3 wa vyakula,mavazi na vinywaji kwa watoto hao ili kuwawezesha kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya 2011.


Amesema kuwa ili kuondoa wimbi la watoto wanaoishi mitaani jamii haina budi ya kuwa inajukumu kubwa la kuwatunza,kuwalea  na kuwawezesha kupata elimu itayowasaidia kujikwamua katika maisha yao ya baadae.
Mh.Kamata ametoa msaada wa mafuta ya kupikia lita 60,Sabuni za kufulia,vinyaji,mchele kilo 200,mbuzi wawili,madaftari kalamu na sukari ambapo pia alishiriki na watoto hao kula nao chakula cha mchana katika kusherehekea mwaka mpya.
Kadharika mbunge huyo ametoa pia msaada wa nguo,Unga wa lishe kwa wafungwa na mahabusu wakiwemo watoto wane ambao mamazao wamo katika gereza la Geita pamoja na kuzungumza na wafungwa na mahabusu wa gereza hilo ambapo amejionea msongamo wa mahabusu unaotokana na kucheleweshwa kwa upelezi wa kesi zinazowakabili.
Aidha kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Geita Joseph Msukuma amesema wilaya hiyo inakabiliwa na ongezeko la idadi ya watoto wanaoishi mitaani hali inayotokana na kuongezeka kwa msongamano wa watu katika Mji wa Geita.
Mwenyekiti ameyataka mashirika hayo yanayolea watoto yatima kufanya jitihada za makusudi kwa kushirikiana na Serikali wahisani na mashirika mbalimbali kuwaondoa watoto walioko mitaani na kuwaweka pamoja ili kuweza kuwalea na kuwapatia elimu itayowasaidia  hapo baadae.
Katika kuunga mkono juhudi za mashirika hao za kulea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu mwenyekiti huyo ametoa msaada wa magodoro 25.Mkoa mpya wa Geita unakabiliwa na ongezeko la watoto wa mitaani ambapo zaidi ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu 2000 wanaishi mitaani kutokana na kuongezeka idadi ambapo zaidi ya watu 100,000 wanaishi mjini Geita.